SOMO: SIFA 7 ZA UCHUMBA
SOMO;Sifa 7 za Wachumba wa Kufanikiwa Kwanza Upo tayari kuingia katika mkataba wa maisha na rafiki yako wa jinsia nyingine? Kabla ya kufaulu kuingia kwenye ndoa, wewe na mwenzio mnapaswa kuwa na sifa za ukomavu zinazoweza kuwahakikishia ndoa imara. Wachumba waliotayari kwa urafiki wa milele huwa na sifa nyingi za kupevuka, lakini kuu kati ya hizo ningependa kushiriki nawe. 1. Kila mmoja anajua anachohitaji na atakachochangia katika ndoa Ni dalili ya utu uzima kung’amua kuwa “si vema” ubakie mwenyewe. Unaonesha umekomaa unapohisi uhitaji wa mwingine maishani mwako ili uwe kamili (Mwanzo 2:18). Unapotambua mahitaji yako ya kihisia, kiroho, kijamii, na hata kimwili unakuwa tayari kumkaribia mwenzako ili ukamilike. Ukiwa na utambuzi huo huoni sababu ya kuficha hisia zako. Huna aibu kufungua moyo wako mbele ya macho ya mwenzako. Unamtaka mwenzio ajue umeanza safari ya kumkaribia ambayo kilele chake ni “mwili mmoja” — ngozi kwa ngozi, moyo kwa moyo (Mwa 2:24-25)...